Kiongozi wa muungano wa Azimio la Umoja One Kenya Raila Odinga jana Jumapili, Agosti 13, 2023 alifanya mazungumzo na seneta Christopher Coons anayezuru Kenya.
Mkutano wa wawili hao unajiri wakati ambapo kuna uvumi kwamba ni sehemu ya juhudi za jumuiya ya kimataifa kupatanisha serikali na upinzani humu nchini.
Taarifa rasmi ya sababu za mkutano huo haikutolewa.
“Ilikuwa furaha yangu kama kawaida kukutana na kubadilishana mawazo na rafiki yangu seneta Coons. Mchana ulikuwa mwema,” alisema Raila baada ya mkutano kati yao.
Mkutano huo ukifanyika siku moja kabla ya kuanza kwa mazungumzo kati ya wawakilishi wa muungano tawala wa Kenya Kwanza na ule wa upinzani wa Azimio la Umoja One Kenya huko Bomas of Kenya.
Hii sio mara ya kwanza kwa Coons ambaye ni mwakilishi wa jimbo la Delaware katika bunge la seneti nchini Marekani kuhusika katika mchakato sawia nchini Kenya.
Baada ya William Ruto kutangazwa mshindi wa urais kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka jana, seneta huyo alikuja Kenya wakati ambapo Raila alikuwa amekataa matokeo ya uchaguzi huo.
Mwaka 2017, alikuwa humu nchini pia baada ya uchaguzi mkuu ambao ulizua mzozo hasa kuhusu uchaguzi wa urais.
Aliongoza ujumbe kutoka Marekani wa kupatanisha rais Uhuru Kenyatta na mshindani wake Raila Odinga na muda mfupi baadaye viongozi hao wawili walipatana kupitia “Handshake”.