Maandamano makubwa dhidi ya utawala wa Rais wa Marekani Donald Trump yamefanyika katika miji mbalimbali kote nchini Marekani katika awamu ya tatu ya mikutano iliyopatiwa jina la “No Kings”.
Waandaaji wa maandamano ya Jumamosi wanakadiria kuwa zaidi ya watu milioni 8 walihudhuria kupinga sera zilizowekwa na Rais Trump.
Wanapinga mambo kama vita vya Iran, utekelezaji wa sheria za uhamiaji na kupanda kwa gharama ya maisha.
Waandamanaji wanamlaumu Rais Trump wakisema anataka kuwatawala kama dikteta, wakimkumbusha kwamba nchini Marekani, mamlaka ni ya watu na wala si ya watu wanaotaka kuwa wafalme au washirika wao matajiri.
Msemaji wa Ikulu ya Marekani aliita maandamano hayo vikao vya matibabu ya wazimu wa Trump na kusema kuwa watu pekee wanaojali ni waandishi wa habari wanaolipwa kuyaangazia.
Jumamosi iliyopita, maandamano yalifanyika katika kila jiji kubwa la Marekani na katika miji midogo na vijiji kote nchini humo na pia katika maeneo nje ya Marekani, kama vile Paris na London.
Mikutano ilifanyika mitaani katikati ya jiji la Washington DC mchana kutwa, huku makundi makubwa ya watu yakitembea katika mji mkuu huo wa taifa.
Kama ilivyokuwa katika awamu zilizopita za maandamano ya No Kings, waandamanaji waliinua sanamu za Trump, Makamu wa Rais JD Vance na maafisa wengine wa utawala, wakitaka waondolewe madarakani na kukamatwa.
Huko Minnesota, ambapo raia wawili wa Marekani, Renee Nicole Good na Alex Pretti, waliuawa na maafisa wa uhamiaji mwezi Januari, maandamano yalifanyika pia Jumamosi.
Vifo hivyo vilizua hasira na maandamano ya kitaifa dhidi ya mbinu za uhamiaji za utawala wa Trump.
Maelfu ya watu Jumamosi walijaza mitaa wakiwa na mabango na pia wanasiasa wengi maarufu wa chama cha Democrat walipanda jukwaani nje ya jengo la State Capitol huko St Paul.
Bruce Springsteen pia alipanda jukwaani na kutumbuiza wimbo wake wa kupinga utekelezaji wa sheria za uhamiaji unaoitwa “Streets of Minneapolis.”