Raia wa Malawi kumchagua rais mpya wiki ijayo huku uchumi ukisuasua

Uchaguzi nchini Malawi umepangwa kufanyika Septemba 16 mwaka huu huku idadi ya wagombea wa urais ikiwa 17. Rais Lazarus Chakwera anatafuta kuchaguliwa kuhudumu kwa muhula wa pili.

Martin Mwanje
2 Min Read
Rais Lazarus Chakwera akifanya kampeni kuelekea uchaguzi wa Septemba 16 / Picha kwa hisani ya REUTERS/Eldson Chagara

Raia wa Malawi watapiga kura kumchagua rais mpya wiki ijayo huku hali ya kiuchumi nchini humo ikiwa ngumu kwa wengi.

Rais wa sasa Dkt. Lazarus Chakwera atatoana kijasho na mtangulizi wake ambaye pia ni mpinzani wake mkuu Peter Mutharika kwenye uchaguzi huo utakaoandaliwa Septemba 16.

Wagombea watatu wa urais kati ya 17 kwenye uchaguzi huo wameshawahi kuhudumu kama rais nchi hiyo na mwingine ni makamu wa sasa wa rais.

Wachambuzi wa mambo wanasema ingawa idadi ya wagombea ni kubwa mno kuliko kawaida, wapiga kura wamepoteza imani kwa wanasiasa kuleta mabadiliko ya kweli kwa nchi hiyo ambayo ni moja ya nchi maskini zaidi duniani.

“Ikiwa ni Chakwera au (mtangulizi wake Peter) Mutharika atakayeshinda, hakuna kitu chochote kitakachobadilika kwetu. Ni kama kuchagua kati ya pande mbili za sarafu moja,” alisema Victor Shawa, mwanamume asiye na ajira mwenye umri wa miaka 23 akiwa katika mji mkuu wa nchi hiyo, Lilongwe.

Shauku iliyokuwepo wakati Dkt. Chakwera akiingia madarakani imedidimia kutokana na kupanda kwa mfumko wa bei ambao umefikia takriban asilimia 30, uhaba wa mafuta na kukithiri kwa ufisadi miongoni mwa masuala mengine.

“Watu wanahisi kunaswa,” alisema Michael Jana, raia wa Malawi na mwanasyansi wa kisiasa kutoka Chuo Kikuu cha Wits nchini Afrika Kusini.

“Uchumi ni mbaya, wanasiasa ni walewale, na raia wengi wa Malawi hawaamini uchaguzi huu utabadilisha maisha yao,” Jana aliiambia AFP.

Chakwera, mwenye umri wa miaka 70 ambaye ni mchungaji wa kiinjili, anatafuta kuchaguliwa ili kuhudumu kwa muhula wa pili.

Website |  + posts
Share This Article