Raia nchini Zimbabwe washiriki uchaguzi mkuu

Tom Mathinji
1 Min Read
Picha/Hisani.

Raia nchini Zimbabwe wanashiriki Uchaguzi Mkuu wakati ambapo taifa hilo linakabiliwa na mfumko wa bei.

Siku hii imetangazwa kuwa siku ya mapumziko ili kuwaruhusu wapiga kura milioni 6.62 waliojiandikisha, kupata nafasi ya kupiga kura ya urais na ubunge.

Rais Emmerson Mnangagwa anakabiliwa na wapinzani 10, akiwemo Nelson Chamisa wa chama kikuu cha upinzani cha Citizens Coalition for Change (CCC).

Mgombea urais anahitaji zaidi ya asilimia 50 ya kura ili kushinda.

Ikiwa hakuna mshindi wa moja kwa moja, duru ya pili ya urais itafanyika baada ya wiki sita.

Huu ni uchaguzi wa kwanza tangu kifo cha Robert Mugabe, ambaye alitawala siasa za Zimbabwe na chama tawala cha Zanu-PF kwa miongo kadhaa.

Alifariki mwaka wa 2019 takriban miaka miwili baada ya kuondolewa madarakani katika mapinduzi ya kijeshi na nafasi yake kuchukuliwa na naibu wake Bw Mnangagwa.

Vituo vya kupigia kura vilifunguliwa saa moja asubuhi, saa za nchi hiyo.

Polisi wamesambazwa kote nchini ili kudumisha amani na utulivu, na idadi yao itaimarishwa na maafisa wa magereza, kulingana na mkuu wa polisi Godwin Matanga.

Share This Article