Maafisa wa usalama wamewakamata raia sita wa kigeni kwenye mpaka wa Kenya na Somalia wakati wakielekea nchini Somalia kujiunga na kundi la wanamgambo la Al-Shabaab.
Sita hao walikamatwa kufuatia hatua ya maafisa kuongeza ushikaji doria kwenye mpaka huo.
Waliokamatwa ni Muhamed Jahad Farah, Saad Suleiman Saleh, Nadrik Mbwana Salum, Abdul Kadir Salum Seif na Ali Issa Ali, wote raia wa Tanzania.
Mwingine aliyekamatwa ni Hassan Tourabih Kintosa raia wa Uganda.
Punde baada ya kukamatwa, sita hao walikiri kuwa walikuwa wakielekea nchini Somalia kujiunga na wanamgambo wa Al-Shabaab.
Ukamataji huo unakuja wiki mbili pekee baada ya raia wengine watatu wa Tanzania kukamatwa katika eneo la Korakora, kaunti ya Garissa baada ya raia kuripoti kwa maafisa wa usalama uwepo wao katika eneo hilo.
Ushirikiano kati ya maafisa wa usalama na wakazi umeshika kasi kaskazini mwa nchi huku wakazi washirikishana taarifa na mamlaka za eneo hilo.
Wakazi wametakiwa kuendelea kukaa macho wakati serikali ikifanya kila juhudi kudumisha amani katika eneo hilo kutokana na hulka ya wanaoshukiwa kuwa wanamgambo wa Al-Shabaab kuwahangaisha wakazi mara kwa mara.