Raia 10 wa kigeni wakamatwa kaunti ya Laikipia

Tom Mathinji
1 Min Read
Raia 10 wa kigeni wakamatwa kaunti ya Laikipia.

Kundi la maafisa wa usalama wa asasi mbali mbali, limewakamata raia 10 wa kigeni waliokuwa wakisafirishwa kuelekea eneo lisilojulikana.

Kumi hao wanaoaminika kuwa raia wa Eritrea, walikuwa wakisafirishwa ndani ya gari aina ya Nissan Vanet, yenye nambari za usajili KCQ 635J katika barabara ya Posta Sipili.

Maafisa hao kutoka idara ya upelelezi wa makosa ya jinai DCI, huduma ya taifa ya polisi na wale wa utawala, walipashwa habari kuhusu gari ambalo lilikuwa likiwasafirisha raia wa kigeni, na kuanzisha msako mara moja.

Kulingana na taarifa ya polisi kutoka kituo cha polisi cha Rumuruti, maafisa hao walipata gari hilo limeegeshwa karibu na kichaka, likiwa na watu wawili ndani, mmoja wao akiwa afisa wa polisi wa kituo cha polisi cha Sipili.

Dereva wa gari hilo alitoweka alipowaona maafisa hao wa polisi.

Aidha maafisa hao pia walipata gari aina ya Toyota Voxy lenye nambari za usajili KBX 580U, lililokuwa likiendeshwa na afisa wa polisi Wilson Nderitu wa kituo cha polisi cha Ol-moran, baada kupekua gari hilo waliwapata raia hao 10 wa kigeni.

Magari hayo mawili yanazuiliwa katika kituo cha polisi cha Rumuruti.

Website |  + posts
Share This Article