Quincy Timberlake akubali mashtaka ya mauaji dhidi yake

Marion Bosire
1 Min Read

Quincy Timberlake mume wa aliyekuwa mtangazaji Esther Arunga amekubali mashtaka ya mauaji dhidi yake katika kesi inayohusu kifo cha mwanao wa kiume.

Timberlake amekuwa kizuizini nchini Australia kwa muda sasa kufuatia kisa ambapo anaaminika kusababisha kifo cha mwanawe.

Mhubiri huyo na ambaye pia aliwahi kuwania urais nchini Kenya alimsababishia mtoto Sinclair madhara baada ya kumgonga kwenye tumbo mara kadhaa katika kile alichokitaja kuwa kufukuza mapepo yaliyokuwa ndani yake. Hayo yalitokea katika makazi yao eneo la Kallangur, Brisbane kaskazini nchini Australia.

Alishtakiwa kwa mauaji Juni 18, 2014. Kesi yake ilifaa kuanza kusikilizwa katika mahakama ya juu ya Brisbane wiki hii lakini akakubali mashtaka dhidi yake.

Awali aliambia maafisa wa usalama kwamba Sinclair alianguka nyumbani kwao ndiposa akapata matatizo ya kupumua.

Mkewe Esther ndiye alifahamisha maafisa wa polisi kwamba mumewe alisababisha kifo cha mwanao kwa kumpiga tumboni mara kadhaa na kumrusha kwenye ukuta.

Esther Arunga hakusaazwa kwani naye alishtakiwa kwa kuwa mshirika katika kisa hicho.

Mashtaka dhidi ya Timberlake yalibadilishwa kutoka mauaji na kuwa kuua bila kukusudia.

Anasubiri kuhukumiwa Septemba 29, 2023.

Share This Article