PSC: Watumishi wengi wa umma wanatumia vyeti ghushi vya masomo

Tom Mathinji
2 Min Read
Watumishi wengi wa umma wanatumia vyeti ghushi vya masomo, kulingana na tume ya kuwaajiri watumishi wa umma PSC.

Tume ya kuwaajiri watumishi wa umma PSC, imebainisha kuwa idadi kubwa ya watumishi wa umma waliajiriwa kutumia vyeti bandia vya masomo.

Mwenyekiti wa tume hiyo Antony Muchiri, alisema wafanyakazi 2,067 wa serikali, wanamiliki vyeti ghushi vya masomo.

Aidha kulingana na katibu huyo, wizara ya usalama wa kitaifa, hospitali ya kitaifa ya Kenyatta, hospitali ya mafunzo na matibabu maalum ya Moi na kampuni ya uzalishaji kawi ya mvuke nchini, ni miongoni mwa taasisi zilizo na wafanyakazi wengi walio na vyeti ghushi vya masomo.

Tume hiyo ya kuwaajiri watumishi wa umma ilisema wafanyakazi wengi walioajiriwa katika hospitali ya kitaifa ya Kenyatta katika kipindi cha miaka kumi iliyopita, walitumia vyeti vya masomo vya kughushi.

Muchiri alisema wafanyakazi hao ni miongoni mwa visa vya vyeti kughushi vilivyogunduliwa katika uchunguzi ulioanza kufanywa mwezi Oktoba mwaka 2022.

Uchunguzi huo ulilenga taasisi 331, miongoni mwazo 52 za serikali, idara na mashirika ya serikali (MDAs), mashirika 239 ya serikali na mashirika ya serikali yanayojitegemea na taasisi 40 za umma.

Akizungumza katika kikao hicho, afisa mkuu mtendaji wa tume ya kupambana na ufisadi Twalib Mbarak, alisema tume hiyo itarejesha mishahara yote na marupurupu yaliyolipwa wafanyakazi waliotumia vyeti ghushi vya masomo.

Matamshi yaliyoungwa mkono na mkurugenzi mkuu wa idara ya upelelezi Amin Mohammed.

Website |  + posts
Share This Article