Mwanamuziki na mwanasiasa wa Tanzania Joseph Haule maarufu kama Profesa Jay amethibitisha kwamba atawania ubunge tena mwaka ujao wa 2025.
Katika mahojiano na mwanahabari Millard Ayo, Jay alisema atatafuta tena kuhudumia watu wa eneo la Mikumi kupitia uchaguzi mwaka ujao.
Ayo alitaka ufafanuzi kutoka kwa Jay kuhusu picha aliyochapisha wiki kadhaa zilizopita kwenye akaunti yake ya Instagram na maneno aliyoandika chini yake.
Kwenye picha hiyo, Haule alikuwa amevaa suti ya rangi nyeusi akiwa na Alex Haule ambaye pia alikuwa amevaa suti nyeusi na kuandika, “Maandalizi ya kurudi mjengoni”.
Jay alikiri kwamba anajiandaa kuwania ubunge kurejelea huduma kwa watu wake, akisema wamekuwa wakimwombea sana apate nafuu na Mungu ametimiza hilo.
Aliwanyoshea kidole cha lawama wafuasi wa chama pinzani ambao anasema walieneza uvumi kwamba amefariki huku wengine wakisema hawezi kuondoka kitandani na hivyo hawezi kuwania uongozi.
Mbunge huyo wa zamani wa eneo la Mikumi alilazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi katika hospitali ya Muhimbili kwa siku 127, na afueni yake inachukuliwa kuwa muujiza.
Mwaka 2015 ndio alichaguliwa uwa mbunge wa Mikumi kupitia chama cha upinzani CHADEMA na akashindwa kwenye uchaguzi wa mwaka 2020.