Prince Indah atangaza harusi yake ya kitamaduni

Hafla hiyo itaandaliwa Jumapili hii na imesababisha afutilie mbali matamasha kadhaa.

Marion Bosire
2 Min Read

Mwanamuziki Evans Ochieng Owino maarufu kama Prince Indah ametangaza kwamba atafanya harusi ya kitamaduni Jumapili hii.

Indah alichapisha picha akiwa na mpenzi wake wa muda mrefu Winnie kwenye akaunti zake za mitandao ya kijamii akisema siku iliyosubiriwa kwa muda sasa imewadia.

“Siwezi kutulia, harusi yangu ya kitamaduni iliyosubiriwa sana na malkia wangu Winnie, hatimaye inafanyika jUmapili hii.” aliandika Indah.

Kufuatia hayo, mwanamuziki huyo alitangaza kwamba amelazimika kufutilia mbali baadhi ya matamasha aliyokuwa amepangiwa kuhudhuria wiki hii ili apate muda wa kujiandaa kwa hafla hiyo.

“Kwa sababu ya hafla hii ya kipekee, tumeamua kufutilia mbali mengi ya matamasha yetu wiki hii ninapojiandaa kwa siku hiyo kubwa.” aliendelea kuelezea kiongozi huyo na mmiliki wa bendi ya Malaika.

Katika miaka ya hivi karibuni, Indah ameinuka kwa kiwango kikubwa katika tasnia ya muziki. Alianza kuimba kwenye bendi ya ROR iliyokuwa ikimilikiwa na Emma Jalamo kabla ya kuwa msanii huru.

Mwaka 2014 alirekodi albamu yake ya kwanza iliyokuwa na nyimbo 6 ambazo ni pamoja na Cinderella, Nyakisumu, Pokna, Uchumi na Ken Soldier.

Oktoba 2016, Prince Indah alirekodi albamu ya pili kwa jina ‘Tenda Wema’ aliyozindua rasmi Disemba 23 mwaka huo.

baada ya hapo aliondoka kwenye bendi ya R. O. R na kuunda yake kwa jina Malaika Ohangla Rhumba – M.O.R.

Website |  + posts
Share This Article