Maafisa wa polisi wamewapiga risasi na kuwaua majambazi wawili, na kupata bunduki moja aina ya AK47 na risasi 15.
Kulingana na idara ya upelelezi wa makosa ya jinai DCI, kundi la maafisa wa polisi kutoka makao makuu ya idara hiyo, lilipelekwa katika kaunti ya Kakamega kukabiliana na kundi moja la majambazi amabalo limekuwa likiwahangaisha wakazi wa Kakamega na maeneo jirani.
Kupitia mtandao wa X, idara ya DCI ilisema baada ya maafisa hao kupata habari za kijasusi kuhusu maficho ya majambazi hao, walianzisha operesheni katika nyumba yao na kuwaamuru majambazi hao kutoka nje, lakini walikaidi agizo hilo na kuwafyetulia risasi maafisa hao.
Ni kutokana na hatua hiyo ndipo maafisa wa polisi waliwapiga risasi na kuwaua. Aidha polisi walisema utambulisho wa majambazi hao bado haujulikani.
Katika nyumba hiyo, polisi pia walipata pikipiki inayoaminika kuwa ya afisa wa polisi ambaye anaendelea kupokea matibabu hospitalini baada ya kushambuliwa na majambazi mjini Butere Novemba 12, 2024.
Miili ya majambazo hao ilipelekwa katika chumba cha maiti katika hospitali ya rufaa ya Bungoma.