Maafisa wa polisi wamewakamata watu sita kwa madai ya ulanguzi wa bangi, katika visa viwili tofauti.
Katika kisa cha kwanza eneo la Merti, maafisa wa usalama waliokuwa wakishika doria kwenye barabara ya Moyale-Isiolo, waliwakamata wahudumu wanne wa uchukuzi baada ya kilo 16.7 za bangi kupatikana ndani ya basi.
Basi hilo aina ya Scania, lenye nambari za usajili KDH 166M, lilikuwa likielekea Nairobi, liliponaswa na maafisa hao.
Na katika mtaa wa Buruburu Jijini Nairobi, maafisa wa polisi walisinasa gari aina ya Toyota Probox baaday ya kulifuata kutoka Ngong na kupata kilo 155 za bangi.
Hata hivyo watu wawili waliokuwa kwenye gari hilo walitoroka, lakini baadaye walinaswa na makachero hao.
Samson Zimbwakale mwenye umri wa miaka 27 na Phesto Sigungu mwenye umri wa miaka 46, walinaswa kutoka maficho yao mtaani Cedar Court, na wanazuiliwa katika kituo cha polisi cha Muthaiga.
Washukiwa hao wanasubiri kufunguliwa mashtaka ya kumiliki na kujihusisha na ulanguzi wa mihadarati.