Polisi watumia vitoa machozi kutawanya wafanyabiashara walioandamana Nairobi

Marion Bosire
1 Min Read

Maafisa wa polisi wamelazimika kutumia gesi ya kutoza machozi kutawanya waandamanaji wafanyabiashara waliofunga barabara za kuingia katikati ya jiji la Nairobi karibu na soko la Marikiti na Muthurwa.

Polisi walikimbizana na wafanyabiashara hao walioamua kuandamana kama njia ya kuonyesha kutoridhishwa kwao na mipango ya kuwahamisha kutoka eneo hilo hadi soko jipya kwenye barabara ya kuelekea Kangundo.

Barabara zilizoathirika zaidi ni ile ya Jogoo na ya Haile Sellasie ambapo waliwasha moto na kuweka mawe kwa hivyo hazingepitika.

Wanabiashara hao ambao huhusika sana na mazao ya mashamba kama viazi, mananasi, vitunguu na machungwa walipatiwa notisi na serikali ya kaunti ya Nairobi Septemba 10, 2024 kwamba wahamie soko hilo jipya mashariki mwa Nairobi.

Agizo hilo ambalo lilistahili kuanza kutekelezwa mara moja, linalenga kupunguza msongamano wa watu na magari na kutoa nafasi kwa maegesho ya magari.

Kaimu katibu wa kaunti Godfrey Akumali amesema soko hilo jipya la Kangundo Road lina nafasi ya kutosha ya kufanya biashara na hata ya maegesho ya magari.

Share This Article