Maafisa wa polisi kutoka kitengo cha ujasusi, DCI wamethibitisha kupokea taarifa za kutoweka kwa Waziri wa zamani Raphael Tuju.
DCI kwenye taarifa yao kwa vyombo vya habari ilikiri kupokea taarifa ya kutoweka kwa mwanasiasa huyo siku ya Jumapili baada ya familia yake kupiga ripoti kwa polisi.
Polisi wamesema gari la Tuju lilipatikana limeachwa kwenye barabara ya Miotoni mtaani Karen, likiwa limewasha taa na kubururwa hadi kituo cha polisi cha Karen.
Uchunguzi unaendelea huku polisi wakiitaka familia kushirikiana nao kufanikisha kupatikana kwa mwanasiasa huyo ambaye pia wakati mmoja alihudumu kama Katibu Mkuu wa chama cha Jubilee.
Maafisa hao wakisema walizuiliwa kuingia nyumbani kwa mbunge huyo wa zamani wa Rarieda mtaani Karen kufanya uchuguzi zaidi.
Kisa hicho kinajiri takriban wiki moja baada ya Tuju kufungiwa na madalali nje ya mali yake inayozozaniwa mtaani Karen.