Polisi wasioweza kutambulika kutoruhusiwa kwa maandamano

Marion Bosire
2 Min Read

Mahakama kuu imeelekeza kwamba maafisa wa polisi wanaotumwa kudhibiti maandamano ni sharti wawe wamevaa sare, nyuso zao ziwe zinaonekana na wasifunike nambari za usajili za magari wanayotumia.

Katika uamuzi aliotoa leo Jumatano Agosti 14 2014, jaji Bahati Mwamuye alielekeza kwamba kulingana na ombi lililowasilishwa na mkurugenzi mtendaji wa chama cha wanasheria nchini LSK, maagizo yametolewa kwa Inspekta Jenerali wa polisi dhidi ya kutuma nyanjani maafisa wasioweza kutambulika.

Jaji Mwamuye ameagiza pia kwamba iwapo maafisa waliovaa kiraia watatumwa nyanjani basi nyuso zao zisifunikwe kiasi cha kutotambulika.

Mwamuye alielekeza washtakiwa wa kwanza wanne wa kesi hiyo ya LSK ambao ni kamanda wa kituo cha polisi cha Central Martin Mbae Kithinji, Isaiah Ndumba Murangiri ambaye ni afisa wa polisi, Moses Mutayi Shikuku afisa mkuu wa kituo cha polisi cha Central na mkuu wa polisi katika eneo la Nairobi Adamson Bungei kuwasilisha majibu yao kwa maelekezo hayo kufikia Agosti 30, 2024.

Murangiri alishtakiwa na LSK binafsi kama afisa wa polisi kwa kile walichokitaja kuwa kumtia mbaroni mmoja wa waandamanaji Hanifa Farsafi kinyume cha sheria kwenye barabara ya Moi Avenue jijini Nairobi ilhali hakuwa na silaha na alikuwa anaandamana kwa njia ya amani.

Bungei na Shikuku walihusishwa kwenye kesi hiyo kutokana na vyeo vyao na mamlaka na hatua ya kutuma nyanjani maafisa wa polisi wasiovaa sare kupambana na watu wanaoandamana kwa njia ya amani.

Inspekta jenerali naye alihusishwa kwenye kesi hiyo kama kamanda mkuu wa maafisa wa polisi.

Share This Article