Polisi wapiga marufuku maandamano ya Chadema, CCM walaani utekaji

Martin Mwanje
4 Min Read

Jeshi la polisi nchini Tanzania limepiga marufuku maandamano yaliyokuwa yamepangwa na chama cha upinzani Chadema kufanyika jijini Dar es Salaam tarehe 23 Septemba 2024.

Msemaji wa Jeshi la Polisi David Misime ametoa onyo kwa viongozi wa Chadema kuacha kuendelea kuwahamasisha wananchi kujihusisha kwa kile alichokiita ni uhalifu

“Jeshi la polisi linatoa katazo kwa yeyote aliyealikwa, kuelekezwa kufika Dar es Salaam kutoka mkoa wowote ule kwa ajili ya maandamano hayo asitubutu kufanya hivyo kwani maandamano hayo ni haramu na hayatafanyika” amesema Misime.

Siku ya Jumatano (11 Septemba 2024), Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe alisema nia ya maandamano hayo ni kudai uhai wa wanachama na viongozi mbalimbali wa chama hicho waliopotezwa.

Hata hivyo Misime ameonya kwamba waliopanga kuhudhuria wasipoteze muda na gharama zao kwani yeyote atakayeingia barabarani atakabiliwa vilivyo kwa mujibu wa sheria za nchi.

th

Chanzo cha picha,CCM

Wakati huo huo Katibu Mkuu wa chama tawala nchini Tanzania CCM Dkt Emmanuel Nchimbi amesema chama hicho kinalaani utekaji na mauaji nchini humo. Dkt Nchimbi amesema mauaji ya hivi karibuni ya kiongozi wa Chadema Mohammed Kibao ni jambo la kusikitisha na linatia hofu kwa wananchi.

“Taifa linapita kwenye mtihani wa hofu miongoni mwa wananchi, na hatuwezi kulipuuza hilo… Mtu yeyote anayehatarisha usalama wa raia, mtu yeyote ama kikundi kinachotekeleza matendo ya utekaji hawawezi kuwa na nia njema na CCM,” amesema Nchimbi.

Awali Mbowe alitoa siku kumi – hadi kufikia tarehe 21 Septemba 2024 – akitaka viongozi husika kuwajibika kwa tuhuma za watu kutekwa na kupotea katika mazingira ya kutatanisha na kuonya hilo lisipofanyika wanachama na viongozi wa Chadema wataandamana.

Hatahivyo, Nchimbi anasema msimamo wa Mbowe na Chadema ni ushindi kwa genge la watekaji. “Tumemsikia Mbowe akitoa mud awa mwisho, yaani tarehe 23 serikali isipotaja majina watachukua hatua. Kwa mtu kama Mbowe kama kafikishwa hapo na genge la watekaji maana yake ni kuwa genge limefanikiwa.”

‘Genge la watekaji lina nia mbaya’

Nchimbi amedai kuwa matendo ya utekaji yanafanya na watu wenye nia mbaya ya kufarakanisha taifa. “Jambo la utekaji na mauaji linatoa taswira mbaya kwa CCM. Hivyo hatuwezi kuunga mkono.”

Nchimbi amasema tayari matendo hayo yanafanya raia wasiwe na imani na polisi, na ameonya hilo likendelea litaathiri usalama na ustawi wa nchi kwa ujumla. “Ni muhimu sisi pamoja na wapinzani kushirikiana ili tusiwape genge la watekaji ushindi. Genge linataka kutufarakanisha.”

Kiongozi huyo amesema CCM inaunga mkono kauli ya rais Samia Suluhu Hassan kutaka uchunguzi ufanyike. “Niseme kuwa CCM imekerwa kweli kweli na jambo hili… Genge hili la watekaji linaweza kuwa popote, ndani ya CCM, polisi au hata Chadema. Muhimu ni kuacha uchunguzi wa kina ufanyike, na majibu yake yapatikane ili hatua zichukuliwe.”

Kuhusu hoja ya Chadema ya kutaka uchunguzi uongozwe na makachero kutoka mashirika ya kijasusi ya kimataifa kama Scotland Yard ya Uingereza, Dkt Nchimbi amesema CCM itaiunga mkono serikali kama itaona umuhimu wa kushirikisha mashirika ya kimataifa.

Hata hivyo, Nchimbi amesema misimamo ya Chadema ya kutaka Rais Samia ang’oke madarakani haiwezekani kwa kuwa yupo madarakani kikatiba na ataondoka pale tu muda wake kikatiba utakapotamatika.

Share This Article