Polisi wanyimwa kibali cha kumkamata Nicki Minaj

Mwanamuziki huyo ameshtakiwa na jamaa ambaye alikuwa meneja wake kwa kile anachokitaja kuwa kumshambulia na anataka fidia.

Marion Bosire
2 Min Read
Nicki Minaj

Maafisa wa polisi wa huko Detroit nchini Marekani wamenyimwa kibali cha kumkamata mwanamuziki Nicki Minaj.

Polisi hao walikuwa wamethibitisha kwamba wameweka ombi kwa afisi ya mkurugenzi wa mashtaka la kutaka waruhusiwe kumkamata mwanamuziki huyo kutokana na tuhuma za kushambulia jamaa aliyekuwa meneja wake.

Afisi ya mkurugenzi wa mashtaka ya Detroit ilithibitisha kwamba ilikosa kutoa kibali hicho kutokana na ukosefu wa ushahidi wa kutosha kuthibitisha makosa ya Nicki Minaj.

Jamaa huyo kwa jina Brandon Jovan Garrett, aliwasilisha kesi mahakamani akidai fidia kwa kutoka kwa Minaj ambaye anasema alimshambulia wakati walikuwa kwa chumba cha kujiandaa huko Detroit, Aprili 21, 2024.

Wakati huo kulingana naye, walikuwa wamemaliza kutumbuiza katika tamasha moja kwenye ukumbi wa Little Caesars, Detroit.

Garrett ametaja pia kampuni ya Minaj iitwayo Pink Personality kama mmoja wa washtakiwa kwenye kesi hiyo.

Anaelezea kwamba siku hiyo alikuwa akirejea kutoka kununua ‘ice cream’ ambayo Minaj alikuwa ameitisha akakutana na mkuu wa usalama wa Minaj ambaye alimtaka afike kwenye chumba cha maandalizi alikokuwa Minaj.

Minaj alikuwa na mkuu huyo wa usalama wake na watu wengine watano wa kundi lake na alikuwa amekasirika na jinsi kazi zilikuwa zinatekelezwa.

Mwimbaji huyo alikasirishwa hasa na hatua ya Garrett ya kupeana jukumu la kumchukulia dawa zake kwa mhudumu mwingine.

Jamaa huyo anasema alijitetea akisema alikuwa na jukumu jingine akalazimika kutuma mtu mwingine kwa sababu alitaka dawa hizo haraka, kisha minaj akamzaba kofi usoni.

Anasema Minaj aligonga pia mkono wake akaangusha stakabadhi alizokuwa amebeba huku akimkaripia kwa maneno makali.

Garrett anasema alijifungia kwenye choo kwa masaa kadhaa kwa usalama wake na kesho yake akapata ujumbe wa kumfahamisha kwamba hakubaliwi kuingia kwenye basi rasmi la uchukuzi wa kundi lao kutoka Detroit hadi Chicago.

Garrett anasema aliarifu maafisa wa polisi wa detroit kuhusu kisa hicho kwa njia ya simu baada ya kuondoka humo, akaarifiwa kwamba alihitajika kurejea huko kuandikisha taarifa.

Alirejea akaandikisha taarifa hiyo kabla ya kurejea nyumbani, Los Angeles. Sasa anataka kesi hiyo iamuliwe na kundi la waamuzi.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *