Maafisa wa polisi katika kaunti ya Kiambu wamenasa pombe haramu katika eneo la Juja.
Pombe hiyo ya thamani ya zaidi ya shilingi milioni moja, ilinaswa baada ya kutolewa habari za kijasusi.
Kulingana na kamanda wa polisi wa kaunti ya kiambu Perminus Kioi, pombe hiyo haramu ilinaswa baada ya wananchi kutoa habari kwa maafisa wa polisi.
Kamanda huyo wa polisi alisema mapipa 250 ya Ethanol ambayo hutumika kutengeneza pombe haramu yalipatikana katika mtaa wa Thome. Vibandiko bandia vya shirika la ukadiriaji ubora wa bidhaa na vile vya halmashauri ya kukusanya ushuru KRA, pia vilinaswa wakati wa oparesheni hiyo.
Alex Mureithi, mwenyekiti wa chama cha wakazi wa eneo hilo, alisema mshukiwa wa pombe hiyo alikodisha nyumba hiyo wiki mbili zilizopita, na wakazi hawakuwa wakifahamu kuhusu shughuli iliyokuwa ikiendelea katika nyumba hiyo.