Maafisa wa polisi wamenasa mbolea na mbegu bandia katika kaunti ya Kakamega, huku washukiwa watatu wakikamatwa wakati wa operesheni iliyotekelezwa Jumatano.
Maafisa wa polisi kutoka kituo cha polisi cha Shianda Mumias Mashariki, walitekeleza operesheni katika nyumba ya Asma Mukoya baada ya kupashwa habari, ambapo walipata lori lililokuwa na magunia 196 ya kilo 50 ya mbolea bandia na kilo 396 ya mbegu bandia za mahindi.
“Baada ya kupashwa habari, maafisa wa polisi walifanya operesheni katika nyumba ya Asma Mukoya mwenye umri wa miaka 38, katika kijiji cha Musoma, kata ndogo ya Lubinu, kaunti ndogo ya Mumias Mashariki na kupata lori lenye nambari za usajili KDL 120K ikiwa na mbolea bandia,’ ilisema taarifa ya Huduma ya Taifa ya Polisi.
Kulingana na taarifa hiyo ya polisi, bidhaa zingine zilizonaswa katika nyumba hiyo ni pamoja na mashini ya kupima uzani, nyuzi za kushona, mashini ya kupakia, magunia matatu ya kilo 50 na mchanganyiko wa magunia yasiyokuwa na chochote ndani.
Washukiwa hao watatu waliokamatwa, wanazuiliwa na polisi, huku wakiwasaidia kwa uchunguzi.
Tukio hilo linajiri huku serikali ikiwaonya wakulima dhidi ya kuingia katika mtego wa kuuziwa mbolea na mbegu bandia.
Huku msimu wa mvua za masika ukiendelea katika sehemu nyingi za nchi, wakulima wamehimizwa kununua mbegu na mbolea zilizoidhinishwa kutoka katika maghala ya Halmashauri ya kitaifa ya Nafaka na Mazao NCPB.