Maafisa wa polisi wamenasa magunia 34 ya mbolea ghushi iliyokuwa ikiuziwa wakulima katika eneo la Koibatek kaunti ya Baringo.
Majasusi wamesema magunia hayo yalikuwa yamepakiwa mawe na mchanga pamoja na mbolea ya kinyesi cha mbuzi.
Polisi wa Eldama Ravine siku ya Ijumaa walipokea ripoti kuhusu watu wawili kutoka kijiji cha Poror waliokuwa wamenunua mifuko 34, ya mbolea hiyo kutoka kwa ghala la halmashauri ya nafaka na mazao NCPB katika kituo cha Eldama Ravine na baadaye kubaini kuwa ulikuwa mchanga na mawe.
Mifuko hiyo ilikuwa na chapa ya mbolea aina ya NPK ambayo huuziwa wakulima na serikali kwa bei ya shilingi 2500 kwa mfuko mmoja.
Kamati ya usalama katika eneo hilo imeagiza kurejeshwa kwa mifuko ya mbolea 2,650 iliyokuwa imeuziwa wakulima kutoka kituo hicho cha NCPB,lakini imekuwa vigumu kwani baadhi ya wakulima walikuwa washaitumia kwa kilimo.