Maafisa wa polisi katika eneo la Juja, kaunti ya Kimabu, wamenasa lita 480 za kemikali aina ya ethanol pamoja na pombe bandia,zilizokuwa zimefichwa katika nyumba moja mtaani Theta.
Pombe hiyo haramu ilitengenezwa, kupakiwa na kuuzwa katika baa za maeneo yaliyo karibu.
Kulingana na kamanda wa polisi kaunti ya Kiambu Michael Muchiri, maafisa hao pia walipata vibandiko vya halmashauri ya kukusanya ushuru, vinavyoaminika vilitumika kuepuka kulipa ushuru na kuwahadaa wateja.
Muchiri aliongeza kuwa, gari lililokuwa limebeba chupa ambazo hazikuwa na chochote ndani, pia lilinaswa.
Wakati wa msako huo, washukiwa wanane, wanawake wawili na wanaume sita, walitiwa nguvuni.
Wakazi waliozungumza na wanahabari baada ya msako huo, walisema shughuli katika jengo hilo hazijakuwa za kawaida, wakidai kuwa huenda usafirishaji wa pombe hiyo haramu hutekeklezwa wakati wa usiku.
Muchiri aliwapongeza wakazi wa eneo hilo kwa kutoa habari kwa polisi, zilizosababisha kufanywa kwa msako huo.