Maafisa wa polisi katika kaunti ya Bomet wamenasa bangi ya thamani ya shilingi milioni moja iliyokuwa ikisafirishwa siku ya Jumatatu.
Akiwahutubia wanahabari, kamanda wa polisi wa kaunti ndogo ya Bomet ya Kati Musa Omari alisema bangi hiyo ilikuwa ikipelekwa Narok na sehemu zingine za nchi.
Omari alisema bangi hiyo ilikuwa imepangwa vyema ndani ya gari aina ya Toyota Noah, ambalo hutumika kusafirisha abiria katika barabara ya Nairobi-Bomet-Kisii.
Inasemekana dereva wa gari hilo aliagizwa na maafisa wa polisi kusimama lakini akakataa.
Magunia manane ya bangi yalipatikana ndani ya gari hilo ambalo limezuiwa katika kituo cha polisi cha Bomet.
Kamanda huyo wa polisi aliwaonya walanguzi wa mihadarati kuwa chuma chao ki motoni, akisema maafisa wa polisi hawatawasaza wanaovunja sheria.