Maafisa wa Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), wamenasa mifuko 41 ya bangi yenye thamani ya shilingi milioni 6.2 katika mtaa wa Komarock Jijini Nairobi.
Kulingana na DCI, dawa hizo zilipatikana kufuatia operesheni iliyotekelezwa kwa ushirikiano wa Kitengo cha Kupambana na dawa za Kulevya (ANU) na Kitengo cha Uhalifu uliopangwa (OSU), katika mtaa wa Komarock Phase 2 Jumapili usiku.
Bangi hiyo yenye uzani wa kilo 205 ilipatikana katika nyumba ya mshukiwa aliyetambuliwa kwa jina Alah Mohamed Kala.
Pia gari aina ya Toyota Noah ambalo liliaminika kutumiwa kusafirisha bangi hiyo, lenye nambari ya usajili KBL 186E, lilinaswa.
DCI iliongeza kuwa Kala ametiwa mbaroni na anatarajiwa kujibu mashtaka ya ulanguzi wa dawa za kulevya. Mamlaka inafuatilia kwa karibu washirika wa Kala.