Maafisa wa polisi leo Jumatano asubuhi walimtia nguvuni kimakosa mwanahabari mkongwe Macharia Gaitho kabla ya kumwachilia huru saa chache baada ya kumzuilia katika kituo cha polisi cha Karen.
Huduma ya Taifa ya Polisi, NPS kupitia mtandao wa X imesema ililenga kumkamata Francis Gaitho anayechunguzwa na huduma hiyo.
“Huduma ya Taifa ya Polisi inafafanua kwamba leo asubuhi, mwanahabari Macharia Gaitho alikamatwa kimakosa, badala ya Francis Gaitho ambaye anachunguzwa,” ilisema NPS katika taarifa.
Huduma hiyo ilielezea kwamba haiwalengi wanahabari kwa vyovyote vile na kuelezea kusikitikia kisa hicho.
“Huduma hii haiwalengi wanahabari kwa njia yoyote, na tukio la leo ni la kusikitisha.”
Awali, familia ya mwanahabari huyo ilidai kuwa Gaitho alikuwa ametekwa nyara na watu ambao hawakujitambulisha.
Bintiye mwanahabri huyo, Anita Gaitho, alisema watekaji nyara hao waliokuwa wakiendesha gari aina ya Toyota Probox lenye nambari za usajili KBC 725J, walimdhulumu baba yake wakati wa kisa hicho.
“Nipo na baba yangu Macharia Gaitho. Amefikishwa katika kituo cha polisi cha Karen. Yuko salama ingawa walimshambulia. Tunapiga ripoti kuhusu utekaji nyara,” alisema Anita katika mtandao wa X.