Maafisa wa asasi mbalimbali za usalama katika eneo la Pwani, wanaendeleza operesheni ya kuangamiza magenge ya wahalifu ambayo yamekuwa yakiwahangaisha wakazi wa eneo hilo.
Huku operesheni hiyo ikionekana kuzaa matunda, washukiwa 51 wanaoshukiwa kuwa wanachama wa magenge ya uhalifu, walikamatwa Jumanne katika kaunti ndogo ya Kisauni, kaunti ya Mombasa.
Kulingana na idara ya upelelezi wa makosa ya jinai DCI, operesheni hiyo ililenga maeneo ya kona Ya Kisauni, Hospitali ya Jocham Barisheba, Sunlight, Mwandoni, Junda, Cobra, uwanja wa Kadongo.
Washukiwa hao waliokamatwa wanadaiwa kuwa sehemu ya magenge almaarufu ‘Panga boys’, ambayo huwashambuliwa wakazi kutumia mapanga na silaha zingine butu, huku wakiwapora mali yao.
Kupitia ukurasa wa X, DCI ilisema kuwa tuk-tuk tano ambazo zinashukiwa kutumika katika wizi wa simu, pia zilinaswa kwenye operesheni hiyo.
Washukiwa hao sasa wanazuiliwa katika kituo cha polisi cha Mjambere,wakisubiri kufikishwa mahakamani.