Huduma ya Taifa ya Polisi, NPS, imetangaza kwamba imeanzisha uchunguzi kuhusiana na kaburi lenye miili mingi lililopatikana huko Kericho.
Katika taarifa, msemaji wa NPS Muchiri Nyaga amesema kwamba tayari maafisa wa polisi wa Kericho wamefika katika eneo la tukio na kulizingira ili kuhifadhi ushahidi.
Muchiri amesema kwamba katika kiwango cha sasa cha uchunguzi huo, wanatafuta kubainisha ukweli kuhusu madai ya kaburi hilo kuwa na miili kadhaa.
Alisema mashahidi waliandikisha taarifa kwa polisi na juhudu zinatekelezwa ili kupata na kuhoji watu zaidi wanaoaminika kuhusika na suala hilo.
“Huduma ya taifa ya polisi inahakikishia umma kwamba suala hili linashughulikiwa kwa umakini wa hali ya juu na utatekelezwa kwa utaalamu na uwazi ili kufichua ukweli,” ilisema taarifa ya NPS.
NPS inaomba umma kuwa na utulivu uchunguzi unapoendelea na kuhimiza yeyote aliye na taarifa zitakazosaidia katika uchunguzi huo kufahamusha polisi karibu nao.
Taarifa hizo zinaweza pia kuwasilishwa kupitia kupiga simu bila malipo kwa nambari 999, 911, 112, 0800 722 203 au WhatsApp kupitia nambari 0709 570 000.
Polisi wa kituo cha polisi cha Kericho walitangaza kwamba walifahamishwa na mwananchi kuhusu kaburi ambalo lina miili mingi katika Makaburi ya Kericho, wakazuru eneo hilo na kupata kaburi jipya.
Mashahidi waliambia polisi kwamba Machi 19, 2026, watu watatu walifika katika makaburi ya Kericho wakitumia gari na kuwasiliana na mlinzi wa ebeo hilo.
Keshoye alfajiri watu hao walirejea wakachimba kaburi ambapo miili 14 ambayo mingine ilikuwa imechanika na mingine ikiwa ndani ya makaratasi ilizikwa.
Mashahidi husika hufanya kazi za kawaida ikiwemo kuchimba makaburi na walihusishwa na watu hao siku hiyo.