Polisi waagizwa kuwawasilisha mahakamani vijana 6 waliotekwa nyara

Martin Mwanje
1 Min Read

Polisi wameagizwa kuwawasilisha mahakamani kesho Jumanne, saa 5 asubuhi, vijana sita waliotekwa nyara siku chache zilizopita. 

Agizo hilo limetolewa na Jaji wa Mahakama Kuu Bahati Mwamuye.

Alitoa uamuzi huo kufuatia kesi iliyowasilishwa na Chama cha Wanasheria nchini, LSK kinachopinga wimbi la utekaji nyara unaoshuhudiwa nchini kwa sasa.

Vijana wanaotakiwa kuwasilishwa mahakamani ni Peter Muteti, Bernard Kavuli na Billy Mwangi.

Wengine ni Gideon Kibet, Rony Kiplangat na Steve Kavingo.

Agizo hilo limekuja wakati shutuma za kupinga ongezeko la visa vya utekaji nyara nchini zikipamba moto.

Idara ya Mahakama, Jaji Mkuu Mstaafu David Maraga, Waziri Mkuu wa Zamani Raila Odinga na kinara wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka ni miongoni mwa wale ambao wamelaani kutekwa nyara kwa vijana na watu wanaodaiwa kuwa maafisa wa polisi.

Inspekta Mkuu wa Polisi Douglas Kanja amekanusa madai ya kuhusika kwa polisi katika utekaji nyara huo.

Kwa mujibu wa Tume ya Kitaifa ya Kutetea Haki za Binadamu, KNCHR, visa 7 vya utekaji nyara viliripotiwa mwezi huu wa Disemba huku watu 6 wakiwa bado hawajulikani waliko.

Idadi ya jumla ya watu ambao bado hawajulikani waliko tangu mwezi Juni mwaka huu sasa imefikia 29.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *