Polisi mmoja kutoka kwenye kikosi cha Kenya alijeruhiwa wakati wa operesheni ya usalama iliyofanywa huko Kenscoff katika eneo la Belot nchini Haiti.
Polisi wa Kenya ni sehemu ya Kikosi cha Kimataifa cha Kudumisha amani nchini Haiti (MSS).
Kwenye taarifa, msemaji wa MSS Jack Ombaka anasema afisa huyo alikimbizwa katika hospitali ya ASPEN Level 2 ili kutibiwa na kwamba hali yake kwa sasa ni thabiti.
“Tunawashukuru raia wa Haiti wenye nia njema na wengineo ambao wamemtakia afisa huyo uponyaji wa haraka,” alisema Ombaka ambaye aliahidi kutoa taarifa zaidi juu ya hali ya afisa huyo baadaye.
Afisa huyo amejeruhiwa mwezi mmoja baada ya afisa mwingine kutoka kikosi cha Kenya kuuawa wakati wa operesheni ya usalama nchini Haiti.
Kifo cha polisi huyo wa Kenya kilithibitishwa na Kamanda wa Kikosi cha MSS Godfrey Otunge.
“Leo, Jumapili, Februari 23, 2025, mmoja wa maafisa wetu wa MSS kutoka kikosi cha Kenya alijeruhiwa wakati wa operesheni katika eneo la SÉGUR – SAVIEN, katika idara ya Artibonite. Afisa huyo alisafirishwa kwa ndege mara moja hadi hospitali ya Aspen Level 2 lakini kwa bahati mbaya, alifariki kutokana na majeraha aliyopata,” alisema Otunge kwenye taarifa wakati huo.
Aifisa huyo aliyeuwa nchini Haiti atazikwa leo nyumbani kwake huko Kajiado.
Kenya imetuma zaidi ya maafisa 900 wa kudumisha amani nchini Haiti ambayo kwa muda imehangaishwa na magenge ya wahalifu.