Polisi Tanzania wafafanua sababu za kumkamata Niffer

Marion Bosire
1 Min Read

Maafisa wa polisi jijini Dar es Salaam nchini Tanzania wameelezea sababu za kumkamata mwanabiashara na mjasiriamali Jenifer Bilikwiza Jovin maarufu kama Niffer.

Kamanda wa Polisi katika kanda maalum ya Dar es salaam Jumanne Muliro amesema kwamba makosa yanayomkabili Niffer ambaye ana ushawishi mkubwa mitandaoni ni pamoja na kuhamasisha wananchi kufanya fujo siku ya uchaguzi.

Katika mahojiano, Muliro aliendelea kuelezea kwamba makosa mengine ya mwanabiashara huyo ni kuhamasisha watu kuchoma vituo vya kuuza mafuta, kuhimiza watu kuwashambulia maafisa wa polisi na vitendo vingine vya vurugu.

Niffer anaaminika kuendesha uhamasisho huo mitandaoni na kupitia njia nyingine ambazo Muliro alisema zitathibitishwa mahakamani.

Haya yanajiri saa kadhaa baada ya polisi hao kudhibitisha kwamba wao ndio walimkamata Niffer kutoka eneo lake la biashara huko Sinza.

Kabla ya hapo, taarifa zilikuwa zimesambaa mitandaoni kwamba mjasiriamali huyo alikuwa ametwaliwa na watu wasiojulikana na kwa sababu zisizojulikana.

Kumekuwa na uvumi unaosambaa nchini Tanzania kwamba kutakuwa na maandamano siku ya uchaguzi mkuu ambayo ni kesho Oktoba 29, 2025.

Website |  + posts
Share This Article