Shehena ya bangi na shillingi milioni 13.4 pesa taslimu, zimepatikana kwenye operesheni ya kijasusi iliyoongozwa na maafisa wa upelelezi kutoka kitengo cha kukabiliana na mihadarati na kile cha kukabiliana na uhalifu wa kimataifa.
Makachero hao wakishirikiana na wenzao kutoka kitengo cha kukabiliana na ugaidi, pia walifanikiwa kuwakamata washukiwa wanne waliokuwa mahali mihadarati hiyo ilipopatikana katika mtaa wa mabanda wa Kariua, ulio viungani mwa eneo la Ngara jijini Nairobi.
Upekuzi wao uliwezesha kupatikana kwa magunia mawili yaliyokuwa na pesa hizo, magunia 26 ya bangi, katoni nne za vifaa vya kusokota bangi, vifurushi 173 vya peremende na katoni moja ya keki zinazoshukiwa kuwa na bangi.
Washukiwa hao Teresia Wanjiru mwenye umri wa miaka 54 na vijana watatu wenye umri wa kati ya miaka 16 na 17 walipelekwa kwa mahojiano huku wakisubiri kufikishwa mahakamani leo Jumatano.