Afisa mmoja wa polisi amehukumiwa kifungo cha miaka 15 jela kutokana na unyanyasaji wa kingono.
Mahakama Kuu mjini Migori ilimhukumu Howard Omwoha mwenye umri wa miaka 37 kifungo hicho baada ya kupatikana na hatia ya kumnyanyasa kingono msichana mwenye umri wa miaka 16.
Wakati huo, afisa huyo alihudumu katika kituo cha polisi cha Rapogi katika kaunti ndogo ya Uriri na anatuhumiwa kutekeleza uovu huo mnamo mwaka wa 2021.
Hakimu Mkuu Mkazi Angela Munyuny alitoa hukumu hiyo akisema Omwoha alikiuka kifungu cha 8(1) (3) cha Sheria ya Kupambana na Dhuluma za Kingono ya mwaka 2006.
Afisa huyo alikabiliwa na mashtaka mbadala ya kushiriki kitendo hicho kiovu na mtoto kinyume cha kifungu nambari 11 cha sheria hiyo.
Omwoha ana siku zisizozidi 14 kukata rufaa.