Afisa wa polisi wa kitengo cha AP amekamatwa kutokana na hatua yake ya kumuua polisi mwenzake kwa kumpiga risasi katika eneo la Mbooni, kaunti ya Makueni Ijumaa.
Mshukiwa Anthony Mariapei na marehemu Hassan Ahmed walikuwa kwenye zamu ya usiku ya kuchunga afisi ya Naibu Kamishna wa kaunti katika eneo la Mbooni Magharibi kisa hicho kilipotokea.
Kilichochochea Mariapei kumuua mwenzake bado hakijabaibika.
Afisa wa polisi ambaye alikuwa kwenye zamu wakati huo katika kituo cha polisi cha Mbooni kilicho karibu na eneo la tukio alisikia milio ya risasi akaarifu wenzake waliokwenda mara moja katika eneo hilo.
Walimpata Ahmed akiwa amechuchumaa bunduki aina ya G3 ikiwa chini karibu naye huku akivuja damu kutoka ubavu wake wa kushoto. Waligundua kwamba alikuwa amepigwa risasi na uhai ulikuwa umemtoka.
Mariapei alijisalimisha katika kituo cha polisi cha Mbooni ambapo anasemekana kukiri kumpiga risasi Ahmed.
Bunduki mbili aina ya G3 zilizokuwa zikitumiwa na maafisa hao wawili siku hiyo zilitwaliwa na moja ilikuwa na risasi 18, nyingine ikiwa na risasi 20.
Mwili wa Ahmed ulipelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali ya kaunti ndogo ya Mbooni Magharibi ukisubiri kufanyiwa upasuaji ili kuchunguzwa.