Polisi ajeruhiwa Kilifi katika vurugu kuhusu mradi wa nyuklia

Alphas Lagat
2 Min Read

Afisa wa polisi leo Jumatano amepata majeraha madogo baada ya vurugu kuzuka eneo la Uyombo katika Kaunti ya Kilifi.

Polisi huyo alijeruhiwa wakati wakazi waliokuwa wakiandamana kulalamikia kutohusishwa kwao katika ujenzi wa mradi wa kuzalisha kawi ya nyuklia kuzua vurugu.

Afisa huyo alikuwa miongoni mwa maafisa wa polisi waliokuwa wameitwa kutuliza hali baada ya wakazi hao kuwasha moto na kuziba barabara zinazoelekea eneo hilo.

Polisi huyo alijeruhiwa katika kichwa chake aliporushiwa kifaa butu. Wakazi kadhaa walijeruhiwa pia katika vurugu hizo.

Wakazi hao walielezea kusikitishwa kwao na Wakala wa Nishati ya Nyuklia (NuPEA) wakisisitiza kwamba hawana uhakika jinsi jamii itanufaika na mradi huo.

“Watu wengi wameumizwa wakati wa maandamano wakiwemo wanawake. Tunataka kuiambia serikali kuwa hatutaki mradi huu wa nyuklia uanzishwe Uyombo,” mmoja wa wakazi hao alisema.

Mkazi mwingine alisema kuwa serikali haijahamasisha jamii juu ya athari inayotarajiwa kutokana na mradi huo.

“Kiwanda kinatarajiwa kujengwa karibu na bahari na tuna uhakika kuwa hakuna kitakachofanyika mradi ukiendelea. Pia tunafahamu wakazi watatakiwa kuhama ili kupisha ujenzi wake,” mkazi mwingine alisema akitoa ombi kwa serikali kushughulikia masuala yanayoleta utata.

“Wakazi wamesema wana suala kuhusu mradi huu na tunaomba serikali ichunguze maswala yao,” mmoja wa waandamanaji aliongeza.

Kiwanda cha Nishati ya Nyuklia (NPP) kilibuniwa kuzalisha megawati 1,000 kufikia mwaka wa 2034 ili kukidhi mahitaji ya nishati ya Kenya yanayoongezeka na kuchochea maendeleo ya viwanda.

Hata hivyo, utekelezaji wa mradi huo umekumbwa na misukosuko kutokana na wasiwasi wa wakazi kuhusu athari zake.

Alphas Lagat
+ posts
TAGGED:
Share This Article