Kampuni ya Kenya Pipeline imemteua Pius Mwendwa kuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wake kufuatia kukamatwa kwa Mkurugenzi Mkuu Joe Sang.
Sang alikuwa miongoni mwa Maafisa watatu Wakuu serikali waliokamatwa baada ya kuhusishwa kwenye sakata ya kuagiza mafuta ya ubora wa viwango vya chini.
Kupitia kwa taarifa siku ya Ijumaa, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa kampuni hiyo Faith Bett, alisema hatua hiyo imechukuliwa kuhakikisha shughuli za kampuni hiyo hazitatizwi baada ya kukamatwa kwa Sang’.
“Bodi hii inafuatilia kwa karibu hali hiyo na inawasiliana na taasisi husika kufahamu zaidi madai yaliyoibuliwa,” alisema Bett kwenye taarifa hiyo.
Wengine waliokamatwa na Sang ni pamoja na Katibu wa maswala ya Petroli Liban Mohamed na Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Kudhibiti Mafuta na kawi (EPRA), Daniel Kiptoo.
Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), iliwahusisha watatu hao na sakata ya uagizaji mafuta yanayodaiwa kuwa ya ubora wa viwango vya chini hapa nchini na kutishia ubora wa mafuta unaouzwa hapa nchini.