Pikipiki inayodaiwa kumsafirisha muuaji wa wakili Kyalo Mbobu yanaswa

Naula aliwaambia maafisa wa polisi kwamba, alikuwa akiendesha pikipiki yenye nambari za usajili KMGL 516L, wakati wa kupigwa risasi kwa wakili huyo mnamo Septemba 9, 2025.

Tom Mathinji
1 Min Read
Pikipiki inayodaiwa kumsafirisha muuaji wa wakili Kyalo Mbobu yanaswa.

Maafisa wa Polisi wamenasa pikipiki inayodaiwa ilitumika kumsafirisha mshukiwa wa mauaji wa wakili Mathew Kyalo Mbobu.

Pikipiki hiyo imepatikana, baada ya maafisa wa upelelezi kuwakamata washukiwa watatu kuhusiana na mauaji hayo, akiwemo Nicholas Lemiso Naula, anayedaiwa kuwa mwendeshaji pikipiki iliyomsafirisha aliyempiga risasi wakili Mbobu.

Alipokuwa akihojiwa, Naula aliwaambia maafisa wa polisi kwamba, alikuwa akiendesha pikipiki yenye nambari za usajili KMGL 516L, wakati wa kupigwa risasi kwa wakili huyo mnamo Septemba 9, 2025.

Polisi walianzisha uchunguzi mara moja wa kuitafuta pikipiki hiyo, na kupitia msururu wa wamiliki wa pikipiki hiyo, maafisa hao waliipata na sasa inazuiliwa kwa uchunguzi zaidi.

“Alipoiona pikipiki hiyo, Naula aliitambua kuwa aliyoitumia kumsafirisha muuaji wa wakili Mbobu.,” ilisema Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), kupitia ukurasa wa X.

Upatikanaji wa pikipiki hiyo unaongeza idadi ya ushahidi, baada ya kukamatwa kwa mshukiwa wa mauaji hayo, waendeshaji wawili wa pikipiki pamoja na pikipiki iliyotumiwa kwenye mauaji hayo.

Kitendawili kilichosalia sasa n kutegua kiini cha mauaji hayo.

Share This Article