Peter Munya afika mahakamani baada ya kibali cha kumkamata kutolewa

Marion Bosire
1 Min Read

Aliyekuwa Waziri wa Kilimo katika serikali ya Rais Uhuru Kenyatta Peter Munya alijiwasilisha mahakamani leo Alhamisi muda mfupi baada ya kibali cha kukamatwa kwake kutolewa kwa kukosa kufika mahakamani kutoa ushahidi kwenye kesi ya mabwawa ya Aror na Kimwarer.

Aliposimama tayari kutoa ushahidi, upande wa mashtaka ulikataa kumhoji ukisema haukuwa tayari kumwongoza katika utoaji wa ushahidi. Upande wa mashtaka ulitaka kesi hiyo iahirishwe.

Lakini Hakimu Eunice Nyutu alikosa kuridhia ombi hilo na hivyo Munya akaachiliwa.

Hakimu huyo alitoa onyo kali kwa yeyote ambaye atajaribu kuvuruga kesi hiyo au kukosa kuwasilisha mashahidi kortini. Alisema iwapo hilo litafanyika, atatumia mamlaka yake kutaja watu hao mahakamani na kuwachukulia hatua kwa kudharau mahakama.

Alisema pia kwamba ni mara ya mwisho kesi hiyo inaahirishwa.

Kesi hiyo itaendelea Septemba 11, 2023.

Share This Article