Peter Kioi ajitetea baada ya kuchangisha pesa mtandaoni kwa shughuli isiyokuwepo

Marion Bosire
1 Min Read

Jamaa kwa jina Peter Kioi ambaye ana ufuasi wa kiwango cha juu kwenye mtandao wa TikTok amejitetea kuhusiana na tuhuma za kuchangisha pesa bila sababu.

Kioi alitangaza kifo cha mwanawe kwenye mtandao wa TikTok ambapo alichangiwa shilingi elfu 180 za kufanikisha mazizi yake lakini ikabainika baadaye kwamba hakukuwa na mtoto aliyekufa.

Akihojiwa kwenye kipindi cha mitandaoni cha Oga Obinna, Kioi alisema hakudanganya wafuasi wake wamchangie bali pia naye alidanganywa.

Kulingana naye mama ya mtoto huyo walikutana naye kwenye TikTok na baadaye akmfahamisha kwamba ana mtoto wake ila hakuwahi kumpa fursa ya kumwona.

Binti huyo alipomfahamisha kuhusu kifo cha mwanao, Kioi mara moja akakitangaza kwenye TikTok na akachangiwa na wanamitandao wenzake.

Anasema alikwenda hadi chumba cha kuhifadhia maiti alichoambiwa maiti ya mtoto wake imewekwa ndiposa akagundua kwamba alidanganywa na hakukuwa na mtoto.

Kwa hasira Kioi alizungumza maneno ambayo yalisababisha Obinna akatize mahojiano akisema hayafai kupatiwa muda.

Kioi alitoa onyo kwa mwanamke yeyote atakehusiana naye kuanzia sasa akisema iwapo mtoto atazaliwa yeye hatawajibika kamwe.

Obinna naye anasikika akimshauri ahakikishe kwamba anatunza wanawe na mama zao iwapo atajipata katika hali kama hiyo.

Website |  + posts
Share This Article