Aliyekuwa nahodha wa timu ya Arsenal Patrick Vieira, ameteuliwa kocha mkuu wa timu ya Genoa inayoshiriki ligi ya Serie A nchini Italia.
Vieira anachukua mahala pa Alberto Gilardino, aliyepigwa kalamu baada ya kuiongoza timu hiyo tangu mwezi Julai mwaka 2022.
Licha ya kuongoza timu hiyo kupanda daraja hadi Serie A, Gilardino anaondoka kutokana na matokeo duni msimu huu, huku Genoa ikiwa na alama 10 baada ya kucheza mechi 12 na inashikilia nafasi ya 17 kwenye msimamo.
Vieira aliyeigura Strasbourg kinachoshiriki katika ligi kuu ya soka nchini Ufaransa mwezi Julai, anapeleka tajiriba yake Genoa hasa baada ya kuifunza kilabu cha Crystal Palace cha Uingereza.
Sasa ataifunza timu kongwe zaidi ya soka nchini Italia, iliyoanzishwa mwaka 1893.
Uteuzi huo wa Vieira pia unampa fursa kukutana na mshambulizi Mario Balotelli, mchezaji ambaye Vieira anamfahamu vyema tangu alipokuwa mkufunzi katika timu ya Nice.