Kiongozi wa kanisa Katoliki ulimwenguni Papa Francis kwa mara nyingine amekashifu mashambulizi yanayotekelezwa na Israel huko Gaza.
Haya yanajiri siku moja tu baada ya waziri wa Israel kumshtumu hadharani kiongozi huyo wa kidini kwa kupendekeza kwamba jamii ya kimataifa inafaa kuchunguza vitendo vya Israel kuona iwapo vinaafiki makosa ya mauaji ya halaiki.
Papa Francis alifungua hotuba yake ya msimu wa Krismasi kwa Makardinali wanaoongoza idara mbali mbali za Vatican kwa kurejelea uvamizi wa Israel wa angani uliosababisha vifo vya wapalestina 25 katika ukanda wa Gaza.
Alitaja mashambulizi hayo ya angani kuwa ukatili na sio vita.
Papa anayeongoza kanisa Katoliki ambalo lina waumini zaidi ya bilioni 1.4 kote ulimwenguni huwa makini sana anapozungumzia mizozo.
Lakini katika siku za hivi maajuzi amekuwa akipaaza sauti kuhusu kampeni ya Israel dhidi ya kundi la waasi wa kipalestina la Hamas.
Israel imekuwa ikishambulia ukanda wa Gaza unaokaliwa na wapalestina tangu Oktoba mwaka 2023 punde baada ya waasi hao wa Hamas kuvamia Israel na kusababisha vifo.
Watu 1200 waliuawa kwenye shambulizi hilo la Hamas juu ya Israel huku wengine zaidi ya 200 wakishikwa mateka.