Pallaso asakwa na polisi kwa kuvamia makazi ya Alien Skin

Uvamizi huo unadaiwa kuchochewa na kutoelewana kati ya wasanii hao wawili wa muziki wakati wa tamasha moja la muziki huko Buloba, katika wilaya ya Wakiso

Marion Bosire
2 Min Read
Pallaso, Mwanamuziki wa Uganda

Maafisa wa polisi jijini Kampala nchini Uganda wanaripotiwa kusaka kundi fulani lililokuwa likiongozwa na mwanamuziki Pallaso linalolaumiwa kwa kuvamia makazi ya mwanamuziki Alien huko Kizungu, Makindye.

Kisa hicho kinadaiwa kutokea Alhamisi Januari 2, 2025 saa tatu asubuhi.

Msemaji wa polisi jijini Kampala Patrick Onyango alithibitisha kisa hicho akikitaja kuwa kosa la wizi na uharibifu na kwamba uchunguzi unaendelea katika kituo cha polisi cha Katwe.

Kulingana na Onyango, Alien Skin ndiye aliwasilisha malalamishi kwa polisi.

Ripoti ya polisi inaashiria kwamba Pallaso na wenzake walikuwa wakitumia silaha kama panga, shoka, nyundo na mawe kutekeleza uhalifu huo.

Inaaminika kwamba uvamizi huo ulichochewa na kutoelewana kati ya wasanii hao wawili wa muziki Alien Skin na Pallaso wakati wa tamasha moja la muziki huko Buloba, katika wilaya ya Wakiso.

Mgogoro huo ulizidi na kusababisha uvamizi wa kwanza wa makazi hayo ya alien Skin saa tisa alfajiri ambapo polisi waliweza kutawanya wavamizi ambao walirejea tena saa tatu asubuhi na kusababisha uharibifu wa mali.

Kulingana na polisi magari matano yaliharibiwa, nyumba tatu zikaharibiwa huku washukiwa wakidaiwa kuiba shilingi milioni sita za Uganda zilizokuwa nyumbani.

Watu wawili waliojeruhiwa kwenye shambulizi hilo wanapokea matibabu katika hospitali ya Mengo huku uchunguzi ukiendelea.

Pallaso ambaye jina lake halisi ni Pius Mayanja ni kakake mwanamuziki Jose Chameleone ambaye anapokea matibabu nchini Marekani.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *