P Diddy akabiliwa na kesi nyingine ya unyanyasaji

Marion Bosire
2 Min Read

Mwanamuziki wa Marekani Sean ‘Diddy’ Combs anakabiliwa na kesi nyingine ya unyanyasaji na kumtumia vibaya mmoja wa washiriki wa kipindi chake cha runinga kilichofahamika kama “Making the Band”.

Mwimbaji Dawn Richard aliwasilisha malalamiko Jumanne katika Wilaya ya Kusini ya New York dhidi ya Combs na wengine wanaohusishwa naye.

Anadai kwamba Combs alinyanyasa wanawake, aliwadhulumu na alikosa kumlipa Richard.

Wakili wa Combs kwa jina Erica Wolff alisema mwanamuziki huyo wa mtindo wa rap alishtushwa na kukatishwa tamaa na kesi hiyo na kutaja madai ya Richard kuwa yasiyo ya kweli.

Anasema mteja wake amesimama kwa ujasiri na ukweli na anasubiri kuthibitisha hilo mahakamani.

Richard alikuwa mmoja wa wanachama wa kundi la wanawake la Danity Kane, lililobuniwa na Combs kupitia kipindi hicho cha Making the Band. Washiriki wa kipindi hicho walikuwa wakishindania fursa kwenye kundi hilo.

Baadaye alijiunga na bendi ya Combs iliyokuwa ikiitwa “Diddy – Dirty Money”.

Richard anasema kwamba alishuhudia Combs akimpiga mpenzi wake wa zamani, Cassandra Ventura mara kadhaa ikiwa ni pamoja na visa vya kutaka kumnyonga.

Hapo ndipo Richard alimshauri Ventura aachane na Combs na akapokea vitisho.

Ventura alimshtaki Combs mwaka 2023 kwa madai ya kumnyanyasa kingono lakini wakaamua kusulisha suala hilo nje ya mahakama ambapo Ventura anaripotiwa kulipwa pesa nyingi.

Kando na unyanyasaji, Richard anamshutumu Combs kwa kutumia talanta yake kama mwimbaji, kumnyima mapato, kuiba kazi zake zilizo na hakimiliki na kumweka kwenye mazingira ya kazi yasiyo ya kibinadamu ambayo ni pamoja na kumpapasa, kumshambulia na kumfunga jela kwa uwongo.

Share This Article