Gavana wa kaunti ya Siaya James Orengo amesema serikali yake imeanzisha mchakato wa kuwaajiri walimu wa shule ya chekechea, ECDE kwa masharti yya kudumu.
“Barua za kuwaajiri zitaanza kutolewa kuanzia Julai 4, 2023,” alisema Gavana Orengo wakati akiahidi kuyapa kipaumbele maslahi ya walimu hao.
Kulingana naye, miaka saba ya kwanza ya ustawi wa watoto ni muhimu kwani wanahitaji mazingira bora na tulivu.
Tangazo hilo linakuja siku moja baada ya serikali ya kaunti ya Kericho kutangaza kuwa itawaajiri walimu 1,115 wa shule ya chekechea kwa masharti ya kudumu kuanzia mwezi Agosti mwaka huu.
Chini ya mpango huo, walimu walio na vyeti katika ECDE watapokea mshahara wa shilingi 25,000; wa stashahada shilingi 35,000, ilhali wale walio na shahada watapokea mshahara wa shilingi 44,000.
Gavana wa kaunti ya Kericho Eric Mutai amesema serikali yake imejitolea kumaliza mateso wanayokumbana nayo walimu hao katika kaunti hiyo kwa sababu ya kulipwa mishahara duni.
Mutai alisema mpango wa lishe ya wanafunzi wa ECDE pia utaanzishwa kuanzia mwezi Agosti.