Waziri mpya wa Ustawi wa Vyama vya Ushirika, Biashara Ndogo na za Kadri Wycliffe Oparanya amemtembelea spika wa bunge la Taifa afisini mwake katika majengo ya bunge jijini Nairobi.
Kulingana na Wetang’ula, yeye na Oparanya walijadiliana kuhusu masuala mbalimbali yanayojumuisha ushirikiano kati ya bunge na Wizara ya Ustawi wa Vyama vya Ushirika, Biashara Ndogo na za Kadri.
Ushirikiano huo utahusu utunzi wa sheria za kufanikisha utekelezaji wa ajenda ya wizara hiyo pamoja na kuhakikisha uendeshaji bora wa serikali katika kuinua taifa hili.
Wawili hao walijadiliana pia kuhusu siasa za eneo la magharibi wanakotoka huku Wetang’ula akisisitiza haja ya viongozi wote kushirikiana kuinua eneo hilo kiuchumi bila kuzingatia miegemeo ya kisiasa.
Kulingana naye, majadiliano hayo yamejikita katika hatua ya Rais William Ruto ya kuunda serikali jumuishi ambapo alichagua mawaziri wanne kutoka upinzani, Oparanya akiwa mmoja wao.