Onyesho la mchekeshaji wa Matekani Jamie Foxx lililopatiwa jina la “Jamie Foxx: What Had Happened Was” litazinduliwa kwenye jukwaa la mitandaoni la Netflix Disemba 10, 2024.
Video ya kutangaza onyesho hilo tayari imetolewa lakini haionyeshi kinachosubiriwa na wengi ambacho ni ufafanuzi kuhusu kilichomtokea kiafya mwaka jana.
Maelezo hayo hata hivyo yanaaminika kuwa kwenye onyesho kamili huku Foxx akisema iwapo atasalia mcheshi basi atasalia hai.
Kwenye video hiyo, Foxx anaonekana akiingia jukwaani kwenye ukumbi uliojaa mashabiki wanaosikika wakimshangilia kisha anatangaza kwamba amerejea na anadondokwa na machozi.
Aprili 11, 2023, Foxx alilalamikia maumivu mabaya ya kichwa yaliyosababisha alazwe hospitalini lakini maradhi aliyokuwa akiugua hayakutajwa.
Mchekeshaji huyo alikaa hospitali kwa muda wa mwezi mmoja kabla ya kuruhusiwa kwenda nyumbani ili kuendelea kupata nafuu.
Julai 2023, Foxx alichapisha video kwenye akaunti yake ya Instagram kuelezea madhila yake akisema alipitia kitu ambacho hakuwahi kudhania kwamba angepitia.
Alisema hakutaka mashabiki wake wamwone akiwa amelazwa hospitalini na kwamba alipitia magumu sana na safari ya kupona haikuwa rahisi.
Mshindi huyo wa tuzo za Oscar na Grammy aliwahi kusema kwamba hakumbuki chochote kutokana na wakati alilazwa hospitalini na kwamba daktari alimwambia kulikuwa na kitu kinafanyika kwenye kichwa chake.