Omtatah aelekea mahakamani, ataka 7 waliotekwa nyara kuachiliwa

Martin Mwanje
2 Min Read
Okiya Omtatah - Seneta

Seneta wa kaunti ya Busia Okiya Omtatah ameelekea katika Mahakama Kuu akiitaka kutoa maagizo ya kuilazimisha Idara ya Polisi na ile ya Upelelezi wa Jinai, DCI kuwasalimisha watu saba waliotekwa nyara, ama wakiwa hai au wamefariki. 

Katika ombi lake kwa Mahakama Kuu mtaani Kibera leo Jumatatu, Omtatah kupitia wakili wake Philip Langat amewashtaki Inspekta Mkuu wa Polisi, DCI na Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma, DPP.

Anawataka maafisa hao kupatiana miili ya Gideon Kibet, Ronny Kiplagat, Steve Kavingo Mbisi, Billy Mwangi, Peter Muteti, Bernard Kavuli na Kelvin Muthoni.

Ikiwa hilo halitafanyika, Omtatah anataka mahakama kuagiza kuachiliwa kwa saba hao kutoka kizuizini.

Seneta Omtatah ameelekea mahakamani wakati ambapo shutuma dhidi ya visa vinavyoongezeka vya utekaji nyara nchini zimeongezeka.

Wa hivi karibuni kulaani visa hivyo anavyosema ni ukiukaji wa sheria ni Jaji Mkuu mstaafu David Maraga.

“Nalaani mauaji, mateso na visa vya utekaji nyara na kutoa wito wa kuachiliwa mara moja kwa vijana ambao bado wanashikiliwa kinyume cha sheria,” amesema Maraga kwenye taarifa yake ya kuwatakia Wakenya heri ya Mwaka Mpya.

“Siasa zetu kamwe hazipaswi tena kufikia kiwango hiki cha ukatili na kutojali.”

Idara ya Mahakama, Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga na Tume ya Kitaifa ya Kutetea Haki za Binadamu, KNCHR ni miongoni waliokashifu jinamizi la utekaji nyara nchini.

Huduma ya Taifa ya Polisi, NPS kwa upande mwingine imekanusha madai ya maafisa wa polisi kuhusika katika utekaji nyara huo.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *