Katibu katika Wizara ya Usalama wa Ndani Dkt. Raymond Omollo, amesema barabara ya kilomita 70 kutoka Ngong hadi Suswa, itapunguza msongamano wa magari ambao hushuhudiwa mara kwa mara kwenye barabara ya Nairobi – Mai Mahiu.
Kupitia kwa taarifa, katibu huyo alidokeza kuwa barabara hiyo ambayo ujenzi wake umekamilika, ni afueni kubwa kwa wasafiri, kwa kuwa itafanikisha kupunguza muda wa usafiri hususan kuelekea Narok, Bomet, Kisii pamoja na Magharibi mwa nchi.
“Barabara hiyo tayari inabuni fursa kadhaa za kiuchumi katika eneo hilo. Wakulima wa kaunti ya Kajiado sasa wanafurahia uchukuzi wa haraka na wa kutegemewa kuelekea katika masoko ya Nairobi,” alisema Dkt. Omollo.
Aidha, alisema barabara hiyo imesababisha kupanda kwa thamani ya ardhi na kuchochea uwekezaji ikiwa ni pamoja na ujenzi wa vituo vya kuuza bidhaa za petroli, vituo vya utoaji huduma, hospitali pamoja na biashara zingine za kando kando ya barabara.
Barabara hiyo inatarajiwa kutekeleza jukumu kuu la kupunguza misongamano ya magari hasaa nyakati za Siku Kuu au nyakati ambapo barabara ya Nairobi- Mai Mahiu inaathiriwa na mafuriko, ajali au maporomoko ya ardhi.