Ombi la kutuma maafisa wa polisi wa Kenya nchini Haiti litawasilishwa bungeni wiki ijayo kama inavyohitajika katika kifungu nambari 240 cha katiba, kwa mujibu wa waziri wa mambo ya ndani Profesa Kithure Kindiki.
Waziri Kindiki anasema serikali haitatumia njia za mkato kupeleka maafisa hao nchini Haiti kulingana na ombi la baraza la usalama la umoja wa mataifa.
Alifichua kwamba baraza la usalama la Kenya lilifanya mkutano Ijumaa na Rais William Ruto ambaye alikuwa mwenyekiti na ni katika kikao hicho ambapo ombi la kuwasilishwa bungeni liliafikiwa.
“Wabunge wanatarajiwa kujadili ombi hilo na kufanya uamuzi kwa kuzingatia maslahi ya nchi hii.” alisema Kindiki akiongeza kwamba kutumwa kwa maafisa hao nchini Haiti hakutapunguza kwa vyovyote uwezo wa maafisa wa polisi kulinda nchi hii.
Alisema polisi wamejukumiwa sio tu kurejesha mifugo wote walioibwa bali pia wanastahili kutambua, kukamata na kushtaki wanaopanga, kufadhili na kutekeleza wizi huo.
Serikali alisema itatetea maafisa wa polisi ambao wanatumia silaha zao kisheria kulinda mali na maisha ya wakenya.
Kindiki alikuwa akizungumza hayo katika shule ya upili ya Kunene ambako aliungana na wazazi, walimu, wanafunzi na viongozi katika mchango.
Baraza la usalama la umoja wa mataifa liliidhinisha wazo lililoanzishwa na Marekani na Ecuador la Kenya kuongoza kikosi cha maafisa wa polisi nchini Haiti kwa mwaka mmoja ili kurejesha utulivu katika nchi hiyo ambayo inatatizwa na magenge yenye silaha kali.