Serikali ya Kenya imeridhia ombi la Benki ya Exim ya India la kutaka Ofisi yake Wakilishi ya Afrika Mashariki iwe jijini Nairobi.
Waziri mwenye Mamlaka Makuu Musalia Mudavadi anasema hatua ya benki hiyo kutaka ofisi hiyo iwe jijini Nairobi ni thibitisho tosha kwamba jiji hilo ni kituo bora cha kibiashara katika kanda hii.
Mudavadi aliisifia benki hiyo akisema awali imetoa usaidizi wa kifedha kwa Kenya katika kusaidia utekelezaji wa miradi katika sekta kama vile za nishati na kilimo.
Aliongeza kuwa katika kipindi cha muda mfupi, benki hiyo itabuni nafasi za ajira kwa Wakenya na kuboresha ujuzi wao katika sekta hiyo.
Katika kipindi cha muda mrefu, ushirikiano kati ya Kenya na benki hiyo utasaidia katika utekelezaji wa miradi ya kitaifa iliyopewa kipaumbele.