ODPP yasema ushahidi unatosha wa kushtaki washukiwa wa mauaji ya Shakahola

Marion Bosire
2 Min Read

Afisi ya mkurugenzi wa mashtaka ya umma nchini ODPP imetangaza kwamba kuna ushahidi wa kutosha wa kushtaki washukiwa 95 wa mauaji ya Shakahola.

Kupitia taarifa ODPP imeelezea kwamba baada ya uchunguzi uliokuwa ukiongozwa na kitengo cha upelelezi wa jinai, faili za uchunguzi ziliwasilishwa kwake.

Baada ya maafisa wa ODPP kudurusu faili hizo, wamepata kwamba ushahidi uliokusanywa unatosha kuwafungulia mashtaka washukiwa hao.

Makosa ya watu hao yameorodheshwa chini ya sheria ambazo ni kanuni ya adhabu sehemu ya 63, sheria ya kuzuia ugaidi ya mwaka 2012 pamoja, ile ya kuzuia uhalifu wa kupangwa ya mwaka 2010, sheria ya watoto ya mwaka 2001, sheria ya kuzuia unyanyasaji ya mwaka 2017 na sheria ya elimu ya msingi ya mwaka 2013.

Wanatuhumiwa kwa mauaji, kuua bila kukusudia, kunyanyasa, kusababishia watu madhara mwilini, kujihusisha na uhalifu uliopangwa, kueneza itikadi kali, kufanikisha vitendovya kigaidi kati ya makosa mengine.

Afisi hiyo ya mkurugenzi wa mashtaka ya umma sasa imeagiza kwamba washukiwa wafikishwe kwenye mahakama kuu au mahakam nyingine ikiahidi kuendesha kesi hizo haraka iwezekanavyo ikitizamiwa kwamba zinafuatiliwa sana na umma.

Shakahola ni eneo la msitu linalopatikana huko Malindi katika kaunti ya Kilifi, ambapo mhubiri tata Paul Nthenge Mackenzie alikuwa akiendesha shughuli zake pamoja na wafuasi wake.

Anasemekana kuhimiza wafuasi wake kufunga kula na kunywa ili wamuone yesu na wengi wakapoteza maisha katika hali hiyo.

Mackenzie aliangaziwa sana mwezi Machi mwaka jana na yeye na wafuasi wake kadhaa wakakamatwa na wamekuwa wakizuiliwa ili kutoa nafasi kwa uchunguzi.

Miili mingi ilifukuliwa kutoka eneo hilo na ilipofanyiwa uchunguzi wengi wa wahasiriwa walibainika kufa njaa huku wengine wakibainika kupoteza maisha kupitia kunyongwa.

Share This Article