Chama cha ODM kimepinga mpango wa serikali kutuma maafisa wa polisi nchini Haiti.
Serikali inapanga kutuma maafisa hao katika nchi hiyo ya Carribean inayokumbwa na ukosefu mkubwa wa usalama.
Hata hivyo, mahakama imesitisha kwa muda utekelezwaji wa mpango huo hadi kesi iliyowasilishwa na chama cha Thirdway Alliance itakaposikilizwa na kuamuliwa.
Kwa upande wake, chama ODM kimeelezea sababu sita kikizitaja kuwa kiini cha pingamizi zake.
Kulingana na chama hicho, maafisa wa polisi wanapaswa kulinda tu usalama wa ndani na wala sio wa nje ya nchi kwa mujibu wa katiba, kuna maafisa wa usalama wasiotosheleza kukabiliana na changamoto ndani ya nchi hususan katika maeneo kama vile Sondu, Lamu na North Rift, na kwamba hali ya usalama nchini salama nchini Haiti ingawa mbaya sio tishio kwa usalama wa taifa la Kenya.
Kadhalika, chama cha ODM kinachoongozwa na Raila Odinga kinasema hatua za awali za kurejesha usalama nchini Haiti hazikuzaa matunda licha ya kuendeshwa na nchi zenye nguvu zaidi duniani, maafisa wa polisi wa Kenya wana rekodi mbaya ya kutetea haki za binadamu, rekodi ambayo haipaswi kunadiwa katika jukwaa la kimataifa na kwamba ahadi ya kuwatuma maafisa wa polisi nchini Haiti ilifanywa hata kabla ya kuidhinishwa na Umoja wa Mataifa na bunge la Kenya.
“Kwa kuzingatia sababu hizi, ODM inatoa wito kwa utawala wa Rais William Ruto kufikiria tena hatua ya kuwatuma maafisa wa polisi nchini Haiti. Tunatoa wito kwa wabunge kupinga hatua hiyo ikiwa suala hilo litawasilishwa bungeni,” kinasema chama hicho katika taarifa.
“Shabaha yetu inapaswa kusalia kutatua changamoto za usalama zinazoikumba nchi hii, kuboresha utekelezaji wa sheria na kulinda maslahi ya polisi na raia wetu.”